Sitisha uhasama miongoni mwa wakimbizi wa ndani Sudan Kusini: UNMISS | | Habari za UN
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS umetoa wito wa kusitishwa mara moja kwa uhasama miongoni mwa wakimbizi wa ndani katika Kambi ya Umoja wa Mataifa ya Ulinzi wa Raia nchini humo kufuatia tukio la jana Alhamis ambapo watu kadhaa waliripotiwa kujeruhiwa na wengine kuuawa.
Video iliyorekodiwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) inaonesha gari la wagonjwa la Umoja wa Mataifa likisindikizwa na walinda amani likipita katika barabara ya vumbi katikati ya umati wa wakimbizi wa ndani katika eneo la Malakal nchini Sudan Kusini.
Kila mmoja aliyefanikiwa kusalia na chochote katika anavyovimiliki, amekibebeba kichwani, mgongoni au mkononi.
Jana muda wa mchana ghasia zilizuka kati ya jamii mbili za wakimbizi wa ndani ambazo zimehifadhiwa katika Kambi ya Umoja wa Mataifa ya Ulinzi wa Raia.
UNMISS inasema vurugu hizo zilichochewa na tukio la kuchomana visu huku ripoti za awali zikitaja raia watatu kuuawa na wengine 20 kujeruhiwa hadi kufikia jana Alhamisi mchana.
Kabla ya hapo, hiyo-hiyo jana Alhamis asubuhi, milio ya risasi ilitanda alfajiri katika mji mkuu wa jimbo la Upper Nile, Malakal, karibu na makazi ya UNMISS.
Walinda amani wa UNMISS waliingia kazini haraka kwa kuwa hali ya wasiwasi imekuwa ikiendelea hapa tangu mwisho wa wiki iliyopita, wakati mzozo katika kituo cha maji uliongezeka haraka na kuwa mzozo kamili ambapo mtu mmoja mwenye umri wa miaka 32 aliuawa.
Kwa kuwa kambi ya walinda amani iko karibu na kambi ya Umoja wa Mataifa ya ulinzi kwa raia, mara zote walinda amani wako chonjo kuchukua hatua ya haraka pindi tu wanapopokea taarifa ya vurugu.
Wakati wa mapigano ya mwezi uliopita, wanajeshi na polisi walinda amani walitumwa mara moja ili kutuliza hali hiyo.
Polisi na walinda amani wa kijeshi kwa sasa wanashika doria ndani ya eneo hilo na kuzunguka eneo la nje, kwa ushirikiano na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Sudan Kusini ili kuondoa hofu miongoni mwa jamii iliyokimbia makazi yao.
Zaidi ya hayo, walinda amani matabibu katika hospitali ya UNMISS wanatoa huduma ya dharura kwa baadhi ya waliojeruhiwa.
Kwa mujibu wa usajili wa kibayometriki wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM), kufikia Desemba mwaka jana 2022, baadhi ya watu 37,032 waliokimbia makazi yao wanajihifadhi katika Eneo la Ulinzi la Umoja wa Mataifa la Malakal.