WFP: Uporaji wa chakula cha msaada Sudan waweka rehami Maisha ya watu milioni 4.4 | | Habari za UN
Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, leo limelaani vikali uporaji katika moja ya maghala yake ya msaada wa kiufundi na chakula Eil Obeid nchini Sudan na kusema uporaji huo unaweka hatarini maisha ya watu milioni 4.4 wanaotegemea msaada wa chakula katika maeneo yaliyoathirika na vita.
Katika taarifa yake iliyotolewa mjini Roma Italia WFP imesema inafanyakazi usiku na mchana ili kuongeza operesheni zake nchini Sudan ili kuwafikia mamilioni ya watu ambao sasa wako katika hali ya sintofahamu na kukabiliwa na njaa kufuatia machafuko yaliyozuka katikati ya mwezi Aprili.
Hivyo limesema “Uporaji huo wa cjakula cha msaada wa kibinadamu na mali zingine za shirika hilo unaweza rehani maisha ya mamilioni ya watu wanaoitegemea WFP kuweza kuishi na pia kuathiri operesheni zetu katika wakati huu muhimu kwa watu wa Sudan, vitendo hivi lazima vikome.”
El Obeid ni mwenyeji wa moja ya kituo kikubwa zaidi cha masuala ya kiufundi cha WFP katika bara la Afrika na kinatumika kama njia muhimu ya operesheni nchini Sudan na Sudan Kusini.
Shirika hilo limeongeza kuwa “Mamilioni ya watu wataathiriwa na shambulio hili la uporaji.”
Ripoti za awali zinaonyesha kuwa vifaa vilivyoporwa katika tukio hilo ni pamoja na chakula na lishe, magari, mafuta na jenereta.
WFP imekumbusha kuwa “Hii si mara ya kwanza kwa chakula na mali za msaada wa kibinadamu za WFP na washirika wetu kuvamiwa na kuporwa. WFP pekee hadi sasa imerekodi hasara inayokadiriwa kuwa ya zaidi ya dola milioni 60 tangu ghasia kuzuka Aprili 15.”
Hivyo WFP imetoa witio kwa pande zote katika mzozo kuhakikisha usalama na ulinzi wa misaada ya kibinadamu , wahudumu wa kibinadamu na mali zao ili kazi yao ya kuokoa maisha iweze kuendelea.
Inakadiriwa kuwa takriban watu milioni 2 hadi milioni 2.5 nchini Sudan wanatarajiwa kutumbukia katika janga la njaa katika miezi michache ijayo kwa sababu ya vita inayoendelea.
Na hali hiyo kwa mujibu wa WFP “Itafanya hali mbaya ya uhakika wa chakula Sudan kufikia viwango vya juu zaidi huku zaidi ya watu milioni 19 wakiathirika saw ana asilimia 40 ya watu wote wa taifa hilo.”