Usambazaji wa Dawa za Kulevya umezidisha mizozo ya kimataifa, ripoti ya UNODC yaonya | | Habari za UN
Kuendelea kwa ongezeko la usambazaji haramu wa dawa za kulevya na mitandao ya usambazaji inayoendelea kukua inazidisha mizozo ya kimataifa na changamoto za huduma za afya na utekelezaji wa sheria, imesema Ripoti ya Dunia ya Dawa za kulevya mwaka huu 2023 iliyozinduliwa leo na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC).
Ulimwenguni kote, zaidi ya watu milioni 296 walitumia dawa za kulevya mwaka 2021, ongezeko la asilimia 23 katika miaka 10 iliyopita imeeleza ripoti hiyo ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na kupambana na dawa za kulevya na uhalifu, UNODC.
Takwimu mpya zinaweka makadirio ya kimataifa ya watu wanaojidunga dawa za kulevya kwa mwaka 2021 kuwa milioni 13.2, asilimia 18 juu kuliko ilivyokadiriwa hapo awali.
Ripoti hiyo inaeleza zaidi kwamba idadi ya watu wanaougua matatizo ya matumizi ya dawa za kulevya imepanda kufikia watu milioni 39.5, sawa na ongezeko la asilimia 45 katika kipindi cha miaka 10.
Vilevile ripoti hii ya UNODC ina ukurasa maalumu kuhusu ulanguzi wa dawa za kulevya na uhalifu unaoathiri mazingira katika Bonde la Amazon kusini mwa Amerika pamoja na sehemu za majaribio ya kimatibabu yanayohusisha dawa zinazovuruga akili na pia matumizi ya matibabu ya bangi; matumizi ya madawa ya kulevya katika mazingira ya kibinadamu; ubunifu katika matibabu ya dawa na huduma zingine; na madawa ya kulevya na migogoro.
Aidha ripoti hiyo ya Dunia ya Dawa za Kulevya pia inaangazia jinsi ukosefu wa usawa wa kijamii na kiuchumi unavyosukuma na pia unavyosukumwa na changamoto za dawa za kulevya; uharibifu wa mazingira na ukiukwaji wa haki za binadamu unaosababishwa na uchumi haramu wa dawa za kulevya; na kuongezeka kwa dawa za kulevya zinazotengenezwa viwandani.
Mahitaji ya kutibu magonjwa yanayohusiana na dawa za kulevya bado hayajafikiwa, ripoti hiyo inaeleza na kwamba ni mtu mmoja tu kati ya watano wanaougua matatizo yanayohusiana na madawa ya kulevya waliokuwa katika matibabu ya matumizi ya madawa ya kulevya mwaka wa 2021, na tofauti zinazoongezeka katika upatikanaji wa matibabu katika maeneo yote ulimwenguni.
Vijana ndio walio hatarini zaidi kutumia dawa za kulevya na pia huathiriwa zaidi na ugonjwa wa matumizi ya dawa katika maeneo kadhaa ulimwenguni. Barani Afrika, asilimia 70 ya watu wanaopata matibabu dhidi ya dawa za kulevya wako chini ya umri wa miaka 35.
Ripoti imeshauri kwamba afya ya umma, kinga, na ufikiaji wa huduma za matibabu lazima zipewe kipaumbele duniani kote vingiunevyo changamoto za dawa za kulevya zitawaacha watu wengi nyuma. Ripoti pia inasisitiza zaidi hitaji la hatua za utekelezaji wa sheria ili kuendana na miundo ya kisasa ya biashara ya uhalifu na kuenea kwa dawa za kulevya za bei nafuu zinazotengenezwa viwandani ambazo ni rahisi kuletwa sokoni.
Akitoa maoni yake kuhusu matokeo ya ripoti hii, Mkurugenzi Mtendaji wa UNODC, Ghada Waly amesema, “Tunashuhudia kuendelea kuongezeka kwa idadi ya watu wanaokabiliwa na matatizo ya matumizi ya dawa za kulevya duniani kote, huku matibabu yakishindwa kuwafikia wote wanaohitaji. Wakati huo huo, tunahitaji kuongeza hatua dhidi ya makundi ya biashara ya madawa ya kulevya ambayo yanatumia mizozo na migogoro ya kimataifa ili kupanua kilimo na uzalishaji haramu wa madawa ya kulevya, hasa ya madawa ya kulevya ya viwandani, kuchochea masoko haramu na kusababisha madhara makubwa kwa watu na jamii.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambao ameutumia kuisihi jamii kutowatenga waathirika wa dawa za kulevya, amehitimisha kwa kusisitiza jumuiya ya kimataifa kuendelea na kazi ya kukomesha matumizi mabaya na ulanguzi haramu wa dawa za kulevya.